Nini maana ya ‘Kuroot’ simu yako? #Android #Rooting

Kuroot ni nini? Kuroot simu ya Android ni
jambo linalofungua geti kuu la programu
endeshaji hiyo na hivyo kukuruhusu kufanya
mambo mengi zaidi katika programu endeshaji
hiyo kuliko ilivyo kawaida.
Tushaulizwa mara kadhaa juu ya jambo hili na
ata baadhi kuuliza jinsi ya kuroot simu zao.
Haya ni yote ya kufahamu kuhusu ‘rooting’.
Kwa kiurahisi
Kama wewe ni mtumiaji wa kompyuta ya
Windows basi utakuwa unafahamu ya kwamba
pale kompyuta ikiwashwa inakupa chaguo la
kuingia kama mtumiaji mkuu yaani
Administrator – ambapo ukiingia kama
Administrator unaweza fanya mengi zaidi
katika upakiaji wa programu na ata katika
masuala ya mafaili.
Pia kuna uwezo wa kuingia kama Mtumiaji
Mgeni – yaani Guest. Ambapo hapa
hautaweza fanya mabadiliko mengi katika
kompyuta hiyo, utabanwa katika mambo mengi
yanayohusu uwekaji programu na ata kufanya
mabadiliko ya mipangilio (settings) ya
kompyuta hiyo.
Toleo la Android katika simu yako – iwe
Samsung, Huawei, Tecno n.k linavyokuja
linakuwa linakupa uwezo wa kufanya
mabadiliko ya kama mtumiaji mgeni (Guest)
katika simu hiyo.
Tendo la kuroot ndilo litakalokupa uwezo wa
mtumiaji mkuu, yaani Administrator katika
simu hiyo na hivyo utaweza fanya mengi ata
yale yanayoweza haribu kabisa programu
endeshaji hiyo.
Je utaweza fanya yapi kutokana na kuroot
simu yako?
Uwezo wa kutumia apps mbalimbali zinazoitaji
ruhusu kubwa unawezeshwa na kitendo cha
kuroot
Ukiroot programu endeshaji ya Android ya
simu yako utaweza kufanya mambo kama vile
Kuweka apps ambazo kwa hali ya
kawaida isingewezekana kabisa
kuwekwa kwenye simu
Kufuta (delete) apps na programu
zilizokuja na simu husika ambazo kwa
kawaida huwa huwezi zifuta. Apps hizi
zinaitwaga Bloatware
Kusasisha au kubadilisha kabisa toleo
lako la Android. Ata kama
mtengenezaji simu husika, iwe
Samsung n.k bado hajakupa sasisho
rasmi kwa ajili ya simu yako kuweza
kupata toleo la kisasa zaidi la Android,
kwa kuroot unaweza fanikiwa kupakia
toleo la kisasa au ata kubadili kabisa
Kufanya mabadiliko mengine
mbalimbali kulingana na utakacho
katika muonekano na utendaji kazi wa
simu yako
Njia za Kuroot
Kuna njia nyingi sana kwa sababu suala la
kuroot simu linategemea mambo mengi sana,
mara nyingi njia ya kuroot simu flani haifanani
na ya kuroot simu nyingine. Tofauti zinakuwa
kwa kampuni kwa kampuni ya simu na ata saa
nyingine tofauti zinakuwa kwa aina ya simu
ata kama zinatoka kampuni moja.
Katika kuroot kwenyewe bila kujalisha app au
programu au hatua utakazotumia, njia kuu ni
mbili;
Ya kutumia makosa ya programu
endeshaji – Kupitia kufahamu makosa,
yaani ‘exploits’ basi watengenezaji apps
au programu wanaweza fanya
programu/app iingie ndani kabisa ya
Android ya simu yako na kukupa uwezo
wa Admin, yaani simu ikawa ‘rooted’
Kwa kuweka ‘Custom Recovery’ – Hii ni
njia isiyo salama zaidi kwa kifaa chako
ila pia ndiyo moja ya njia inayokuwa
mara nyingi tofauti tofauti kwa kila
kifaa.
Muhimu kufahamu
Makampuni yenyewe ya simu sio
yanayotoa njia za kuroot na kwa kiasi
kikubwa huwa hawashauri ufanye
jambo hili. Kama simu ina warranty
basi kitendo cha kuroot kitaondoa sifa
ya warranty hiyo.
Ukikosea njia au ata kama umefanya
kila kitu sahihi kama mambo
yasipoenda vizuri basi Android inaweza
nasa katika hali inayoifanya simu yako
isiweze tumika. Hali hii inaitwa ‘Brick’ –
yaani jiwe. Mara nyingi hii inamaanisha
itakubidi uanze upya.
Tutakuletea njia mbalimbali maarufu za kuroot
simu lakini kama unajiamini na unataka fanya
mwenyewe basi mtandao wa XDA ni moja ya
sehemu muhimu ya kuanzia. Kitu muhimu
sana ni kuhakikisha unafuata maelekezo na
kutumia mafaili husika kama maelezo ya jinsi
ya kuroot simu hiyo husika. Njia hazifanani.
Je ushawahi kuroot simu yeyote? Waambie
wengine ilikuwa ni simu gani na ulitumia njia
gani?

Previous
Next Post »

Ads Inside Post