Ukosefu wa mfumo wa kuondoa maji taka Shinyanga watishia kutokea mlipuko wa kipindupindu.

Katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Bw.Abdul
Dachi amemuagiza mkurugenzi wa mamlaka ya
maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga
Eng.Sylvester Mahole kuhakikisha mfumo wa
uondoaji wa maji taka katika mji huo unajengwa
na kuanza kutumika haraka iwezekanavyo
kwakuwa ukosefu wa miundombinu hiyo
unachangia kutokea mlipuko wa magonjwa ya
matumbo mara kwa mara ikiwemo ugonjwa wa
kipindupindu.
Kauli hiyo imetolewa na katibu tawala wa mkoa
wa Shinyanga Bw.Abduli Dachi katika ziara ya
kushtukiza aliyofanya katika ofisi za mamlaka ya
maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga
ambapo alibaini changamoto kadhaa
zinazokwamisha mamlaka hiyo kutoa huduma
bora kwa wananchi.
Katika hatua nyingine katibu Dachi ametembelea
ofisi za bonde la maji kanda ya kati na
kushtushwa na mrundikano wa vyuma chakavu
na majengo yaliyochakaa katika eneo hilo
ambapo alilazimika kutoa amri ya kuondolewa
vyuma hivyo ili kupisha nafasi kwa ofisi za
mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira
Shinyanga kuhamishia ofisi zake katika maeneo
hayo.
Awali kabla ya maagizo ya katibu tawala
mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa
mazingira mkoani Shinyanga Eng.Sylvester
Mahole ameeleza baadhi ya changamoto
zinazokwamisha mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja
na baadhi ya taasisi za serikali kutolipia ankara
za maji na uhaba wa watumishi na vitendeakazi.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post