Rais Magufuli alaani kuuawa kwa Rubani Roger Gower

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amelaani kitendo cha watu wanaosadikiwa kuwa
ni majangili kumuua kwa kumpiga risasi Rubani
wa helkopta Roger Gower, raia wa Uingereza na
kisha kuidondosha helkopta aliyokuwa
akiiendesha.

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Jumanne
Maghembe akiwa eneo la tukio ilipotunguliwa
helkopta ya TANAPA iliyomuua Kept. Roger
Gower.

Tukio hilo limetokea wakati alipoungana na Askari
wanyamapori waliokuwa wakikabiliana na
majangili katika pori la akiba lililopo katika wilaya
ya Meatu Mkoani Simiyu.
Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa sana na
tukio hilo na ameitaka Wizara ya Maliasili na
Utalii kuhakikisha waliomuua Rubani Gower na
kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha
wanakamatwa na wanafikishwa mikononi mwa
vyombo vya sheria.
Amemtumia salamu za pole, Balozi wa Uingereza
hapa nchini kwa kumpoteza raia wake ambaye
alikuwa akitoa mchango mkubwa katika kuhifadhi
wanyamapori wa hapa nchini Tanzania.
Aidha, Rais Magufuli amesema serikali yake
itahakikisha inaendeleza mapambano dhidi ya
ujangili kwa nguvu zake zote na kuwataka
wananchi na wadau mbalimbali wa hifadhi ya
wanyamapori, kutokatishwa tamaa na tukio hili
na watoe ushirikiano wa kutosha kuwafichua
watu wote wanaojihusisha na ujangili ama
biashara ya bidhaa zitokanazo na ujangili.
Katika tukio hilo, pamoja na kumuua Rubani
Roger Gower watu hao wanaosadikiwa kuwa
majangili wamemjeruhi Askari wanyama pori
mmoja na wamewaua tembo watatu.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post