Rais Dkt.Magufuli akutana na katibu mtendaji wa Afrika Mashariki Richard Sezibera Ikulu DSM.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Magufuli amekutana na kufanya
mazungumzo na katibu mtendaji wa jumuiya ya
Afrika Mashariki Dkt. Richard Sezibera Ikulu jijini
Dar es Salaam ambapo amepokea taarifa ya
maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi wa
jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe
02 Machi, jijini Arusha.
Rais Magufuli ndiye mwenyekiti wa sasa wa
jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi
tano wanachama ambazo ni Tanzania, Kenya,
Uganda, Rwanda na Burundi.
Akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo
katibu mtendaji wa jumuiya hiyo Dkt. Richard
Sezibera, amesema maandalizi kuhusiana na
mkutano huo yanakwenda vizuri.
Amesema pamoja na mambo mengine mkutano
huo, utajadili masuala kadhaa yakiwemo mpango
wa kuanzisha viwanda vya magari ndani ya
jumuiya ili kupunguza uingizaji wa magari kutoka
nje ya nchi na marais kuzindua pasi ya kusafiria
ya jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kuhusu hali ya jumuiya, Dkt. Sezibera amesema
inaendelea vizuri na ametaja baadhi ya mambo
ambayo yamefanyika kuwa ni kutiwa saini kwa
mkataba wa umoja wa forodha, makubaliano ya
soko la pamoja na makubaliano ya sarafu moja.
Mengine ni kuwepo kwa mazungumzo kuhusu
uimarishaji wa miundombinu kama vile reli na
umeme ndani ya jumuiya, na mazungumzo
kuhusu umoja wa kisiasa.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje,
ushirikiano wa Afrika Mashariki, kikanda na
kimataifa Dkt. Augustine Mahiga, amesema
Tanzania ikiwa ni mwenyeji wa kikao hicho ipo
tayari kupokea ugeni na kwamba pamoja na
kufanyika kwa kikao hicho, marais wa Tanzania
na Kenya watafungua barabara inayounganisha
Tanzania na Kenya katika mpaka wa Holili na
kutakuwa na shughuli ya kuweka jiwe la msingi
katika kituo cha pamoja cha mpakani kwa ajili ya
kuwezesha upitaji wa mizigo na watu yaani "One
stop boarder post"

Previous
Next Post »

Ads Inside Post