› Wakuu wa shule za sekondari Mwanza wavuliwa madaraka kwa tuhuma za ubadhirifu.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo
amevunja bodi ya shule ya sekondari Pamba
iliyopo jijini Mwanza na kumvua madaraka mkuu
wa shule hiyo Aidan Dotopery pamoja na walimu
wengine wawili kutokana na kushindwa
kusimamia vyema matumizi ya fedha na mali za
shule zao.
Walimu wengine waliovuliwa nyadhifa zao na
mkuu huyo wa mkoa ni pamoja na mkuu wa
shule ya sekondari Nyakurunduma January
Luganyika na mwalimu mkuu wa shule ya msingi
Nyamagana Masau Mtakilolwa.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mkuu huyo
wa mkoa wa Mwanza kufanya ziara katika shule
hizo na kuonyesha kutoridhishwa na mazingira ya
uwekezaji kwenye vitega uchumi vya shule ya
sekondari ya Pamba, huku baadhi ya nyaraka
pamoja na mikataba ambayo shule hiyo imefunga
na wafanyabiashara hao ikiwa imegubikwa na
utata.
Mwalimu January Ruganyika ambaye aliwahi
kuwa mkuu wa shule ya sekondari Pamba kabla
ya kuhamishiwa sekondari ya Nyakurunduma,
ameshushwa madaraka yake baada ya
kugundulika kuwa hakuwa makini katika
kuhakikisha mali za shule hiyo pamoja na fedha
zinatumika kwa manufaa ya shule na sio kukuta
mikataba mibovu na yeye kuamua kuiendeleza
bila kutafuta ufumbuzi wake.
Kwa hali hiyo mkuu huyo wa mkoa amemuagiza
mkurugenzi wa jiji la Mwanza kuwapangia vituo
vingine vya kazi kama walimu wa kawaida kwa
kushindwa kuwajibika katika nyadhifa zao na
kutekeleza majukumu yao kikamilifu, huku mkuu
wa shule ya sekondari Pamba Aidan Dotopery
akilazimika kujenga hoja za utetezi.
Lazaro Nyambura, mmoja wa walimu wa shule ya
sekondari Pamba ameiomba serikali kuingilia kati
sakata hilo katika kutafuta kiini cha tatizo la
shule hiyo kwani wahusika walionufaika na miradi
hiyo wapo salama salimini lakini wanasababisha
mateso kwa walimu wengine ambao
wanalazimika kutumikia adhabu isiyo wastahili.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post