Wahariri wa Mawio wachiwa, Lissu kuhojiwa leo

Kwa ufupi
Waliachiwa jana saa 6.40mchana
baada ya kukamilisha masharti ya
dhamana ya kuwa na wadhamini
wawili kila mmoja ambao walisaini
hati ya Sh20milioni.

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam jana imewaachia
kwa dhamana Mhariri wa gazeti la
Mawio, Simon Mkina na Mhariri wa
gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrissa
baada ya kuwashikilia tangu juzi.
Wakati wahariri hao wakiachiwa,
imeelezwa kuwa Mwanasheria Mkuu
wa Chadema, Tundu Lissu ametakiwa
kufika polisi leo kwa mahojiano
dhidi ya tuhuma zinazowakabili
Mkina na Idrissa. Mbunge wa
Ubungo, Saed Kubenea na wakili wa
kujitegemea, Peter Kibatala
wamesema Lisu anatarajia kuhojiwa
leo na polisi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Simon Sirro alipoulizwa kuitwa kwa
Lissu alisema hana taarifa hizo lakini
Lissu mwenyewe alisema ameitwa na
kwamba leo mchana atakwenda.
Mkina na Idrisa walijisalimisha juzi
mchana katika Kituo cha Polisi cha
Kati baada ya kutakiwa kufanya
hivyo kwa madai ya kuandika habari
za uchochezi ambako walihojiwa
kwa saa nane. Waliachiwa jana saa
6.40mchana baada ya kukamilisha
masharti ya dhamana ya kuwa na
wadhamini wawili kila mmoja
ambao walisaini hati ya Sh20milioni.
Wadhamini hao ni Robert Katula,
Michael Sarungi na Josephat Isango.
Wakili wa wahariri hao, Peter
Kibatala alisema ni busara kuwapa
muda polisi kufanya uchunguzi.
Mkina alisema wamehojiwa na
wametakiwa kuripoti kituoni hapo
kila siku saa mbili asubuhi hadi hapo
kesi yao itakapoisha. Idrissa alisema
baada ya kujisalimisha, askari
walianza kumhoji kuhusiana na
habari iliyoandikwa katika gazeti la
Mawio yenye kichwa cha habari
Machafuko yaja Zanzibar.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post