SERIKALI YAKANUSHA UZUSHI UNAOENEZWA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII KUMHUSU RAIS MAGUFULI

Hivi karibuni kumejitokeza uzushi
unaosambazwa katika mitandao ya kijamii ya
ndani ya nchi na nje ya nchi kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
amefukuza wageni kutoka nje waliokuwa
wanafanyabiashara zao nchini kwa kuwa
serikali yake haitaki wageni kufanya biashara
nchini.
Serikali haijafukuza wageni kutoka nje ya
nchi kufanya biashara nchini na haina
mpango wa kuwafukuza wageni wanaoishi
nchini kwa vibali vilivyotolewa kisheria na
Idara ya Uhamiaji.
Uzushi huo usiokuwa na ukweli umeenezwa
kufuatia Idara ya Uhamiaji kutekeleza jukumu
lake la kufuatilia wageni wote wanaoishi
nchini bila vibali halali vya ukaazi ambapo
kwa mwezi Novemba na Desemba mwaka
2015 wageni 372 walioondoshwa nchini.
Kazi ya kufuatilia wageni wanaoishi nchini
bila vibali halali vya kisheria haijaanza katika
Serikali ya Awamu ya Tano. Idara ya
Uhamiaji nchini tangu Januari hadi Desemba
mwaka jana iliondosha nchini jumla ya
wageni 1,642 waliokuwa wanaishi na kufanya
shughuli zao nchini kinyume na Sheria.
Uzushi unaoenezwa hauna ukweli wowote na
hauna nia njema na nchi yetu kwani kati ya
mwaka 2014 na 2016 Idara ya Uhamiaji
imetoa vibali vya ukaazi (Residence
Permits) 40,765 kwa wageni wawekezaji na
wafanyabiashara, wageni wanaofanyakazi za
kuajiriwa, wageni wanaokuja kwa ajili ya
Masomo, matibabu, dini, utafiti na wastaafu
kuishi na kufanya shughuli zao nchini.
Serikali inawakaribisha wageni kuja nchini
kuwekeza na kufanya shughuli zao kwa
kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.
Aidha, kuna uzushi unaenezwa kuwa Rais
Dkt John Pombe Magufuli amepiga marufuku
wanawake kuvaa nguo fupi kama njia ya
kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa
wa UKIMWI.
Mheshimiwa Rais tangu aingie madarakani
hajawahi kuagiza wala kutoa tamko
kuhusiana na uzushi wa kukataza uvaaji wa
nguo fupi ili kupunguza maambukizi ya
Ukimwi kama inavyoenezwa katika mitandao
ya ndani na Nje ya Nchi ambayo inanukuu
habari hiyo kuwa imeandikwa na Gazeti la
Kenya “The Standard”
Serikali inapenda kuutangazia umma kuwa
uzushi huo unaomhusu Mheshimiwa Rais
Magufuli umetungwa na watu wasioitakia
mema nchi yetu kwa lengo la kumdhalilisha
Rais na hauna ukweli hivyo watu wasishiriki
kuueneza kwa njia yeyote ile.
Serikali kupitia balozi zake za Kenya na
Afrika Kusini zinafuatilia chanzo cha uzushi
huu kuhusu Rais Magufuli kwa kushirikiana
na nchi husika na watakaobainika kutunga na
kueneza uzushi huu watachukuliwa hatua za
kisheria.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post