TCRA iyabane makampuni ya mitandao ya Simu juu ya vifurushi vya UNLIMITED

Moja ya shirika kubwa la mawasiliano nchini Marekani, T-Mobile limekubali kulipa dola milioni 48 za Kimarekani (takribani Tsh bilioni 100) kutokana na ulaghahi kwa wateja wao juu ya vifurushi vya intaneti visivyo na vikomo – ‘UNLIMITED’.
Shirika hilo lilibanwa na mamlaka ya usimamizi wa masuala ya mawasiliano nchini Marekani (FCC) chombo chenye mamlaka ya usimamizi unachoweza kukilinganisha moja kwa moja na TCRA kwa Tanzania.
Suala limenifanya pia kuomba TCRA waliangalie kwa hapa kwetu kwani tayari kuna mitandao mingi ya simu inayopiga kelele za vifurushi vya UNLIMITED vya intaneti na huku ndani yake kuna usiri mkubwa wa kile utakachopata baada ya kulipia kifurushi hicho.
Mara nyingi mitandao ya simu huwa wanabana kasi ya huduma ya intaneti kwenye vifurushi vya ‘UNLIMITED’.
Kosa la T-Mobile katika vifurushi vya UNLIMITED vya intaneti ni nini?
FCC (Federal Communications Commission) waliikuta kampuni ya T-Mobile na hatia katika uchunguzi wao ulioonesha mtandao huo wa simu
haukuwa wazi kwa wateja wake kuhusu vipingamizi vya kasi na kiwango cha data unachoweza kutumia katika vifurushi vyao vya ‘UNLIMITED’ .
Mkurugenzi wa T-Mobile, Bwana John Legere
Suala hili ni kwa mitandao mingi sana Tanzania lipo, mitandao imekuwa ikija na vifurushi vya UNLIMITED/visivyo na VIKOMO vya intaneti lakini kiukweli vina vikomo vingi tuu – mfano; kasi kushushwa baada ya kutumia kiwango flani cha data, n.k.
Nakumbuka HALOTEL walivyoanza kutoa huduma mwanzoni nilijiunga kifurushi cha UNLIMITED cha intaneti huku wakihahidi ya kwamba kasi itapungua kidogo baada ya mimi kutumia kiasi flani cha data; ila ukweli ni kwamba kasi ilipungua kiasi cha huduma ya intaneti kutofanya kazi kabisa. Sijui kama kuna mabadiliko yeyote hadi sasa.
Huko nchini Marekani hii si mara ya kwanza kwa kampuni ya simu kujikuta katika kikaango kutokana na kutumia neno ‘UNLIMITED’ kwenye vifurushi ambavyo haviendani na ukweli neno hilo. Tayari kampuni nyingine kubwa AT&T imepigwa faini ya dola milioni 100 mwaka 2015 (takribani Tsh bilioni 218).
Ipo mitandao ya simu yenye vifurushi vya UNLIMITED vya intaneti vya kweli; yaani kuanzia kasi hadi kiwango cha data utakachotumia. TCRA wabane wote wanaopiga kelele za ‘vifurushi vya UNLIMITED’ ilihali ni uongo…waache kutumia neno hilo pale ambapo haliendani na kile ambacho mteja atapata…..kwani kufanya hivyo ni udanganyifu na hadi sasa wamekuwa wakiufanya muda mrefu sana. TCRA wachukue hatua.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post