Serikali imewasimamisha kazi watendaji wawili
kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia
leo, ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta
bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita
kwa zaidi ya miaka mitano.
Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha
Makatibu Wakuu kilichofanyika leo Februari 12,
2016 ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara,
Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za
kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.
“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za
kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Katika
kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote
hadi uchunguzi utakapokamilika, pia utafute mtu
wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,”
alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena
Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari,
Bi. Bernadina Mwijarubi, ambaye ndiye
anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.
Pia Waziri Mkuu amesema ofisi yake
itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi,
ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika
kuwa walihusika, hatua rasmi zitachukuliwa na
iwapo itathibitika hawakuhusika basi
watarudishwa.
Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji
mafuta kwa kutumia flow meters uendelee
kutumika, na ule upimaji wa kukadiria uache
kutumiwa mara moja.
Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu
alifanya ziara kukagua flow meters za zamani
zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha
akatembelea na kukagua flow meters mpya
ambazo zinajengwa Kigamboni, amabazo
zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na
sh. bilioni 12.96/- za sasa).
EmoticonEmoticon