Simba yakaa kileleni ligi kuu, Kiiza aking'ara

Mabao mawili ya mshambuliaji mganda, Hamisi
Friday Kiiza [Diego] yametosha kuipa Simba SC
ushindi wa bao 2-1 dhidi ya wenyeji, Stand United
katika mchezo wa mkali wa ligi kuu ya Tanzania
Bara jioni ya leo uwanja wa Kambarage mjini
Shinyanga.
Kwa ushindi huo, Simba SC inapanda kileleni
mwa ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu huu,
ikifikisha pointi 45, baada ya kucheza mechi 19,
ikiwazidi kwa pointi mbili, mabingwa watetezi,
Yanga SC ambao hata hivyo wana mchezo
mmoja mkononi.
Aidha, Simba SC watalazimika kuiombea ‘dua
mbaya’ Azam FC katika mchezo wake wa kesho
dhidi ya Coastal Union uwanja wa Mkwakwani,
Tanga iendelee kubaki kileleni.
Azam FC itaingia kumenyana na Coastal kesho,
ikiwa na pointi 42 ikimaanisha kuwa wakishinda
kwa wastani mzuri wa mabao watarejea kileleni.
Kiiza alifunga mabao yake katika dakika za 34 na
47, hivyo sasa anaongoza kwa kufunga ligi kuu
akifikisha mabao 16 dhidi ya 14, ya mshambuliaji
wa mahasimu wao, Yanga SC, Mrundi Amissi
Tambwe.
Stand United ilipata bao lake la kufutia machozi
dakika ya 90 kupitia kwa David Ossuman.
Hata hivyo, kama Simba itashinda mechi yake
dhidi Yanga wikiendi ijayo, maana yake itakuwa
ni mbio kali za kileleni kati ya Simba na Azam FC
na kuiacha Yanga.
Mechi nyingine za ligi kuu leo, katika dimba la
karume jijini Dar es Salaam wenyeji JKT Ruvu
wametoshana nguvu na Kagera Sugar kwa sare
ya bao 1-1.
Katika dimba la Sokoine jijini Mbeya wenyeji
Mbeya City wamewavurumisha
wanakishamapanda Toto Africans ya Mwanza
kwa bao 5-1 , Mkwakwani Tanga wenyeji
Mgambo Shooting waliangukia pua baada ya
kukubali kichapo cha bao 1-0 toka watanga
wenzao African Sports.
Na katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini
Mtwara wenyeji wanakuchele Ndanda FC
wamewazamisha wanalizombe majimaji ya
Songea kwa kichapo cha bao 1-0.
Ligi hiyo inataraji kuendelea tena hapo kesho
kwa michezo miwili kupigwa katika viwanja
tofauti, huku kila timu ikisaka point tatu muhimu
ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo
wa ligi hiyo.
Mjini Shinyanga wenyeji wachimba migodi ,
Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Tanzania
Prisons kwenye uwanja wa Mwadui Complex,
huku Coastal Union wakiwaalika Azam FC
kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Wakati huo huo mara baada ya kuhitimishwa kwa
michezo ya mwisho ya makundi ya ligi ya soka
daraja la kwanza Tanzania bara na kuibuka utata
wa matokeo ya michezo iliyohusisha timu
zilizokuwa zikiwania nafasi ya kupanda daraja
kwenda ligi kuu Tanzania bara shirikisho la soka
nchini limefanya maamuzi yafuatayo kabla
yakutangaza nani kapanda.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
halitatangaza timu iliyopanda Ligi Kuu msimu
ujao kutoka Kundi C, mpaka itakapoamuliwa na
vyombo husika vya TFF baada ya michezo ya
kundi hilo kuchezwa leo jioni katika viwanja
tofauti nchini.
TFF imefikia hatua hiyo ili kupata nafasi ya
kupitia taarifa za michezo kati ya JKT
Kanembwa v Geita Gold na Polisi Tabora v JKT
Oljoro iliyochezwa leo jioni katika mikoa ya
Kigoma na Tabora.
Taarifa za michezo hiyo kutoka kwa wasimamizi
husika na vyanzo vingine vinakusanywa ili
zifanyiwe kazi na vyombo husika vya TFF.
Katika michezo hiyo ya leo, Geita iliibuka na
ushindi wa mabao 8 – 0 dhidi ya JKT Kanembwa,
huku Polisi Tabora wakiibuka na ushindi wa
mabao 7 – 0 dhidi ya JKT Oljoro.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post