Serikali imesema itachukua hatua kali kwa
kampuni ya Halotel kama itashindwa
kutekeleza makubaliano ya mkataba wa
kusambaza huduma za simu na mtandao
katika ofisi za Serikali katika kila Wilaya
nchini kote.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.
Makame Mbarawa wilayani Maswa wakati
akizungumza na watendaji wa sekta ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mkoani
Simiyu na kusisitiza kutoa ushirikiano
unaostahili kwa kampuni hiyo.
“Makubaliano yetu kati ya Serikali na Halotel
ni kuunganisha ofisi za Umma kwa mtandao
zikiwemo shule tatu katika kila Wilaya,
Hospitali, Mahakama na Ofisi za Polisi ili
kuwezesha mkakati wa mawasiliano vijijini
kutekelezeka”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa ameeleza kuwa ifikapo
mwaka 2017 kila eneo hapa nchini litakuwa
na huduma ya mawasiliano ya mtandao na
kuwezesha wananchi wote kunufaika na
huduma hizo.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa
amekagua Ujenzi wa Barabara ya Lamadi-
Bariadi KM 71.8 na Bariadi-Maswa KM 49.7
na kuwapongeza makandarasi wanaojenga
barabara hizo kwa kazi nzuri wanayofanya.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya,
hakikisheni kazi yenu inauwiana na thamani
ya fedha na kuhakikisheni wafanyakazi
wazawa wanapewa kipaumbele katika kazi
wanazoziweza na kupewa mikataba stahiki
ya kazi wanazozifanya”, amesititiza Prof.
Mbarawa.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amemuagiza
mkandarasi anaejenga barabara ya Maswa-
Mwigumbi KM 50.3 kuhakikisha nyumba
zinazojengwa kwa ajili ya mkandarasi
zinajengwa kwa ubora ili zitumike kwa muda
mrefu.
“Nakuagiza Meneja wa TANROADS,
hakikisha nyumba hizi baada ya mradi wa
barabara kukamilika unazikabidhi kwa jeshi
la polisi ili waweze kuzitumia kwa ajili ya
makazi na ofisi”, amesema Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu Bw. Eraston Mbwilo amemwomba
Waziri Prof. Mbarawa kuelekeza nguvu za
ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi
katika mkoa huo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya
Maswa Bi. Rosemary Kirigini amemuomba
Waziri Prof. Mbarawa kuwawezesha Wakala
wa Majengo nchini (TBA) kukamilisha mradi
wa Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo
unaojengwa sasa kwa miaka mitano ili
kuipunguzia Wilaya hiyo adha ya kutumia
jengo chakavu ambalo si salama hasa
kipindi cha mvua.
Waziri Prof. Mbarawa pia amekagua Kiwanja
wa Ndege kilichopo Mkoa wa Shinyanga na
ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)
kiwanjani hapo na kusisitiza kuwa Serikali
iko katika hatua za kuboresha uwanja huo
kuwa wa kisasa ili kuvutia mashirika mengi
ya ndege kutumiwa kiwanja hicho.
Waziri Prof. Mbarawa yupo kwenye ziara ya
kukagua miradi ya ujenzi kwenye sekta za
barabara, nyumba, viwanja vya ndege na
mkongo wa taifa wa mawasiliano katika
mikoa ya kanda ya ziwa ambapo
ametembelea Wilaya za Busega, Bariadi na
Maswa mkoani Simiyu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Makame Mbarawa (aliyevaa koti la
bluu), akisikiliza maelezo ya mkandarasi
kuhusu ujenzi wa mtambo (hauonekani
pichani) wa kusaga kokoto kwa ajili ya
ujenzi wa barabara ya Maswa-Mwigumbi Km
50.3.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Makame Mbarawa, akiongea na
vibarua wanaofanya kazi kwenye mradi wa
barabara ya Maswa-Mwigumbi Km 50.3,
mkoani Simiyu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Makame Mbarawa akiongea na
wafanyakazi wa sekta za Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano kuhusiana na mkakati wa
Wizara wa kuongeza mapato mkoani Simiyu
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon