Polisi waomba JWTZ kusaidia vita dhidi ya majambazi

Dar es Salaam. Siku moja baada ya
majambazi kuvamia Benki ya Access
Tawi la Mbagala Rangi Tatu, kuua
watu watatu akiwamo Polisi na
kujeruhi watu wengine watatu
akiwamo polisi, Waziri wa Mambo
ya Ndani, Charles Kitwanga amesema
wataomba msaada wa Jeshi la
Wananchi (JWTZ) ili kukabiliana na
matukio ya ujambazi.
Alisema Jeshi la Polisi linajipanga
upya kuhakikisha wananchi
wanakuwa na amani kwa
kuwashughulikia majambazi popote
walipo.
Waziri Kitwanga alisema wanaanza
na Mkoa wa Pwani, kwa kuhakikisha
wanawasaka na kufyeka mapori yote
ya Bagamoyo na kwingineko ili
kuvunja mtandao wao.
“Kama walidhani Jeshi la Polisi
limelala lipo macho, walichofanya ni
kama wamemuamsha aliyelala,
tutawasaka, tutawakamata na
tutawapeleka kwenye mkono wa
sheria na tutahakikisha
tunawamaliza wote,” alisema
Kitwanga.
Alisisitiza kuwa wanaotumia pikipiki
nguvu ya ukaguzi itaongezwa dhidi
ya vyombo hivyo, kwa sababu
inaonekana wahalifu wengi hasa
majambazi hutumia usafiri huo
kutekeleza uovu wao.
Akielezea tukio la uporaji wa
Mbagala, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Simon
Sirro alisema wamefanikiwa kuwaua
majambazi watatu kati ya 12
waliofanya uvamizi huo.
Alisema majambazi hao walikufa
baada ya kupigwa risasi katika
majibizano ya risasi na Polisi katika
Kijiji cha Chui Mkuranga, baada ya
kujaribu kutoroka walipozidiwa
nguvu.
Alisema majambazi hao wakiwa na
pikipiki sita, huku kila moja ikiwa na
majambazi wawili waliokuwa na
bunduki aina ya SMG na mabomu ya
kutupa kwa mkono, walivamia benki
hiyo na kuwashambulia kwa risasi
kisha kuwajeruhi wafanyakazi wa
benki hiyo waliokuwa katika chumba
cha kuhifadhia fedha.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni
Salum Juma na Francis Amani, na
kupora kiasi cha fedha
kinachokadiriwa kuwa kati ya Sh20
na 30 milioni za kaunta baada ya
kushindwa kuvunja chumba cha
kuhifadhia fedha.
Alisema kabla ya kuingia ndani,
walivamia kibanda cha walinzi na
kumpiga risasi askari mwenye
namba H7739PC Khalid Juma
ambaye alifariki dunia papo hapo.
Pia, walimjeruhi kwa kumpiga risasi
kwenye nyonga askari Shaban,
ambaye amelazwa katika Hospitali
ya Muhimbili na kupora bunduki
mbili.
Kamanda Sirro alisema majambazi
hao baada ya kufanya uporaji
walipokuwa wanaondoka, walifyatua
tena risasi iliyompata kidevuni na
kumuua papo hapo Abdi Salum,
ambaye ni muuza duka jirani na
benki hiyo na Baraka Fredrick,
mlinzi wa kampuni ya Security
Group of Africa.
“Hata hivyo Polisi wamefanikiwa
kukamata bunduki tatu kati ya hizo
mbili ni mali ya Polisi, mabomu
matatu ya kutupa kwa mkono na
pikipiki sita zilizokuwa zikitumiwa
na majambazi hao walipozidiwa
nguvu walizitelekeza na kukimbia,”
alisema Sirro.
Katika hatua nyingine, Februari 18,
eneo la Kiwalani polisi walikamata
majambazi watatu wakiwa na
bastola moja na Februari 24 eneo la
Upanga karibu na Daraja la
Sarender, askari waliwakamata
watuhumiwa watatu kwa makosa ya
kujihusisha na ujambazi wa kutumia
silaha.
Kamanda Sirro alisema baada ya
kuwahoji walikiri kufanya matukio
ya ujambazi wa kutumia silaha na
kumtaja mtuhumiwa mwenzao
mmoja anayeishi Tabata Kinyerezi
jijini Dar es Salaam.
“Alipofuatwa nyumbani kwake,
alikutwa na sare za jeshi hilo, redio
ya upepo na pingu,” alidai kamanda
huyo.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post