1. Utangulizi
Kumekuwepo na taarifa kupitia vyombo
mbalimbali vya habari vya Kitaifa na Kimataifa
kuhusu Homa ya Zika ambao ni ugonjwa
unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama
“Zika Virus”. Ugonjwa huu uligundulika kwa mara
ya kwanza nchini Uganda katika miaka ya 1947
kwenye wanyama aina ya sokwe/nyani (rhesus
macaque) ndani ya Misitu ya Zika, karibu na
Ziwa Victoria. Mnamo mwaka 1952, ugonjwa wa
zika uligundulika kwa binadamu nchini Uganda na
Tanzania, na mwaka 1968 uligunduliwa nchini
Nigeria. Kuanzia mwaka 1951 hadi 1981, ugonjwa
huu umeshatolewa taarifa katika nchi takribani
sita (6) za Afrika ambazo ni Afrika ya Kati,
Egypt, Gabon, Sierra Leone, Tanzania na Uganda.
Vile vile, ugonjwa huu umeshatolewa taarifa
katika nchi za India, Indonesia, Malaysia,
Philipine, Thailand na Vietnam na pia nchi za
Amerika na Pacific.
Kuanzia mwezi Mei 2015, ugonjwa huu ulianza
kutolewa taarifa ambapo hadi sasa umeathiri
zaidi Bara la Amerika ya Kusini. Kuna takribani
nchi 22 ambapo Wagonjwa wamethibitishwa
kimaabara kuwa na ugonjwa wa Zika. Nchi hizo
ni Brazil (Majimbo 14 yameathirika), Colombia,
Suriname, El Salvador, Guatemala, Paraguay,
Mexico, Venezuela, Panama, Cape Verde,
Honduras, Panama, France (French Guiana na
Martinique, United States of America (Puerto
Rico), Guyana, Barbados, Ecuador, Bolivia, Haiti,
Ujerumani, France (Saint Martin and Guadeloupe
na Dominican Republic.
Ugonjwa huu unaenezwa na mbu aina ya Aedes
ambaye (huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na
pia nyakati za mchana/jioni). Aina hii ya kirusi
ipo katika familia ya “Flavirus” ambapo pia wapo
virusi vya ugonjwa wa Dengue, Homa ya Manjano
(Yellow Fever), Japanese ancephalitis na West
Nile Virus.
Kirusi cha homa ya Zika kama kile cha Dengue
kinaambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine
kwa kuumwa na mbu wa jamii ya Aedes hasa
Aedes aegypti. Mbu huyu anaishi katika
mazingira ya makazi ya binadamu, huuma wakati
wa mchana ndani ya nyumba au kwenye maeneo
yenye viwili, hususani majira ya asubuhi na jioni
kabla ya jua halijazama. Mbu huyu anazaliana
katika maji yaliyotuama hasa kwenye vyombo vya
nyumbani, makinga maji ya paa za nyumba,
matairi ya gari, ndoo, makopo nk.
2. Dalili za Homa ya Zika
Dalili za ugonjwa huu zinafanana na za homa ya
Dengue, ambazo ni homa, kuumwa na kichwa,
maumivu ya viungo, macho kuwa mekundu na
vile vile kupata vipele vidogo vidogo kama harara
(Skin rashes). Dalili hizi huanza kujitokeza
kuanzia kati siku ya 2 hadi 7 tangu mtu
alipoambukizwa kirusi cha homa ya Zika.
Uko uwezekano, ambao haujathibitishwa rasmi,
kwamba wakati mwingine wagonjwa wanaweza
kupata matatizo katika ubongo (Neurological
Complications) na miguu kupooza (Gullein Barre
Syndrome), na wajawazito huweza kujifungua
watoto wenye ulemavu wa kichwa yaani kichwa
kuwa kidogo kulingana na umri wa mtoto
(microcephaly).
Kwa wakati mwingine dalili za ugonjwa huu
zinaweza kufanana sana na dalili za malaria.
Hivyo basi, natoa rai kwa wananchi kuwa, wakati
wanapojisikia homa au wamepata homa
wahakikishe wanapima ili kugundua kama wana
vimelea vya malaria au la, kwa kuwa dalili za
ugonjwa wa Zika zinaweza kufanana sana na
dalili za malaria.
Homa ya Zika inaweza kutibika kama mgonjwa
atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa
matibabu ya haraka. Hakuna dawa maalum ya
ugonjwa huu wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa
kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa
huu kama vile homa, kupungukiwa maji na damu.
3. Ugonjwa wa Homa ya Zika haujaingia
Tanzania
Mara tu baada ya kuwepo kwa taarifa juu ya
ugonjwa huu, Serikali kupitia Wizara ya Afya
imefanya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika vituo
vya kutolea huduma za afya nchini pamoja na
mipakani kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa
magonjwa (surveillance system ya Wizara).
Tumejiridhisha kuwa ugonjwa wa homa ya Zika
kwa sasa haujaingia nchini kwetu. Hivyo,
Wananchi wasiwe na hofu ila waendelee
kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu pamoja
na magonjwa ya Dengue na Malaria kwa ujumla
ikiwa ni pamoja na kuzingatia yafuatayo:-
(i) Kuangamiza mazalio ya mbu kwa:
kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au
kunyunyizia viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya
mbu kwenye madimbwi hayo.
kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka
mazalio ya mbu kama vile; vifuu vya nazi,
makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa
hovyo, nk.
kufyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya
watu.
Kuhakikisha kuwa maua yanayopandwa
kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji
kutuama.
kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko
imara.
kusafisha gata za paa la nyumba ili
kutoruhusu maji kutuama.
(ii) Kujikinga na kuumwa na mbu kwa;-
Kutumia viuatilifu vya kufukuza mbu
“mosquito repellants”.
Kuvaa nguo ndefu ili kujikinga na kuumwa na
mbu.
Kutumia vyandarua vilivyosindikwa viuatilifu
(kwa wale wanaolala majira ya mchana hasa
watoto).
kuweka nyavu kwenye madirisha na milango
ya nyumba za kuishi.
4. Hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ni
pamoja na:-
.
1. Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa
Shirika la Afya Duniani (WHO) inaendelea
kuwasiliana na kushirikiana kwa karibu na Shirika
la afya Duniani – Ofisi ya Tanzania kwa lengo la
kupata Taarifa na maelezo zaidi ya kukabiliana
na ugonjwa huu. Kamati ya Dharura ya Miongozo
ya Kimataifa ya Afya ya WHO yaani
“International Health Regulations Emergency
Committee” itakutana siku ya Jumatatu ya
tarehe 1/2/2016, mjini Geneva,Uswisi ili kufanya
tathmini ya ugonjwa huo na kutoa tamko na
maelekezo zaidi ya namna ya kudhibiti Ugonjwa
huu kwa nchi wanachama.
Baada ya tamko/Mwongozo huo wa WHO, Wizara
ya Afya itaandaa Taarifa ya tahadhari ya
ugonjwa huu kwa ajili ya kusambazwa kwa
Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya
Tanzania Bara. Aidha, taarifa hii itajumuisha
namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa
(ainisho la Ugonjwa), “Ukweli Kuhusu
Ugonjwa” (Fact Sheet), Mwongozo kwa
watumishi wa afya wa namna ya kuchukua
sampuli. Vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya
kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu
vitatolewa.
2. Wizara itaanza kutoa elimu kwa wananchi
kupitia Radio na Runinga kuhusu ugonjwa huu
sambamba pia na ugonjwa wa Dengue ambao
uambukizi wake unasababishwa na Mbu aina ya
Aedes.
3. Kuendelea kutoa vyandarua vyenye uatilifu
katika Mkoa yote Tanzania ili kufikia lengo la
asilimia 95.
4. Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika
vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na
mipakani kupitia mfumo wa surveillance ya
Wizara. Aidha, Wizara inatoa maelekezo kwa
Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya hapa nchini
kutoa taarifa za watoto watakaozaliwa wakiwa
na ulemavu wowote wa kichwa ikiwemo
“microcephaly” au “anencephaly”.
5. Kufuatilia kwa karibu ongezeko la wagonjwa
wenye homa isiyokuwa ya malaria kwa Mikoa na
Wilaya zote nchini ili kuweza kufanya uchunguzi
wa kina iwapo kuna ugonjwa huu.
6. Kuimarisha uwezo wa kutambua ugonjwa huu
kwa kina kupitia maabara ya Taifa iliyopo katika
Taasisi ya uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMR). Wizara itashirikiana na wadau
mbalimbali wakiwemo Shirika la Afya Duniani
(WHO) na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (Centre
for Disease Control (CDC) katika kuhakikisha
kuwa vitendanishi vya kutambua ugonjwa huu
vinapatikana.
7. Kushirikisha program ya Malaria na NIMR
katika kudhibiti mbu kwa kupulizia na kunyunyizia
viuatilifu. Hii inalenga kuangamiza mbu wapevu
na viluwiluwi.
5. Hitimisho
Ugonjwa wa Homa ya Zika bado haujaingia
Tanzania. Wananchi waondoe hofu juu ya uwepo
wa ugonjwa huu. Hata hivyo, ni muhimu kwa kila
mmoja wetu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi
ya magonjwa ya Zika, Dengue na malaria ambayo
huenezwa kwa namna inayofanana.
Aidha, mvua hizi kubwa zinazoendelea kunyesha
hapa nchini zinaweza kuchangia kuongezeka kwa
mazalio ya mbu. Hivyo, utupaji, uzoaji na uhifadhi
wa taka katika vijiji na miji yetu ni lazima
uimarishwe katika kuhakikisha mazingira yetu
yanakuwa salama kwani bila ya kuzingatia hayo,
tunatoa fursa kwa mazalio ya mbu kuongezeka
na hata kuwa karibu zaidi ya makazi ya
binadamu.
Wizara ya Afya itaendelea kutoa taarifa za mara
kwa mara kwa wananchi ili waweze kuelewa
kuhusu ugonjwa huu na kuchukua hatua stahiki.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon