Dar es Salaam. Mabalozi wa nchi
zinazounda Umoja wa Ulaya (EU)
wameeleza kusikitishwa na kitendo
cha Tume ya Uchaguzi (ZEC) wakati
mazungumzo ya kutatua mgogoro
yakiendelea na kumtaka Rais John
Magufuli kutumia nafasi yake ya
uongozi kutatua mtanziko wa kisiasa
visiwani Zanzibar.
Taarifa ya pamoja iliyotumwa kwa
vyombo vya habari na mabalozi hao
jana, pia inamtaka Rais Magufuli
kuendeleza wito wake wa kuzitaka
pande zote zitafute suluhu kwa
amani.
Tamko hilo limetolewa siku saba
baada ya mwenyekiti wa ZEC, Jecha
Salum Jecha kutangaza kuwa
uchaguzi wa rais wa Zanzibar,
wawakilishi na madiwani utarudiwa
Jumapili ya Machi 20, lakini siku
tano baadaye CUF ilitoa tamko la
kutoshiriki uchaguzi huo wa
marudio.
Kutokana na sakata hilo, mabalozi
hao wamelaani kitendo hicho
wakisema kurudia uchaguzi kwa
kigezo kuwa utaratibu ulikiuka,
kinawatia wasiwasi kwa kuwa tume
hiyo haikutoa ushahidi wa ukiukwaji
huo.
Mabalozi hao wamesema katika
tamko lao kuwa ZEC imerudia kauli
yake ya kuwa uchaguzi ulikiuka
taratibu licha ya waangalizi kutoka
EU, Jumuiya za Afrika Mashariki,
Sadc Marekani na Jumuiya ya
Madola kufanya tathmini na
kujiridhisha kuwa ulikuwa huru na
haki.
“Tunasikitika kuwa ZEC imetangaza
tena kuwa uchaguzi utarudiwa
Zanzibar, wakati mazungumzo baina
ya pande mbili yanaendelea. Kwa
manufaa ya Watanzania wote,
tunasisitiza kuwa hali ya kisiasa ya
visiwani humo ni bora ikatatuliwa
kwa pande mbili kukubaliana,”
inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliyotumwa kwa
ushirikiano wa mabalozi wa
Uholanzi, Norway, Hispania, Italia,
Ujerumani, Finland, Ufaransa,
Sweden, Uswisi, Uingereza, Ireland
na Marekani inasisitiza kuwa
kitendo cha upande mmoja kuamua
kurudia uchaguzi, kinaweza
kuzidisha hofu na taharuki miongoni
mwa Wazanzibari.
“Tunawaomba Wazanzibari kuwa
watulivu na wavumilivu nyakati hizi
na tunazitaka pande zote mbili na
washirika wao kuendelea kufanya
kazi pamoja ili wapate suluhisho la
amani,” ilisema taarifa hiyo.
Pia inasema ili uchaguzi uwe wa
kuaminika, mchakato wake hauna
budi kuziwakilisha pande zote na
kuwa huru na wa haki.
Hata hivyo, mabalozi hao wamesema
kulingana na mazingira ya Zanzibar
kwa sasa, itakuwa vigumu kwa
waangalizi wa kimataifa kutegemewa
kushiriki kwa namna yoyote katika
uchaguzi huo.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon