Google watambulisha simu mpya, zifahamu Google Pixel na Pixel XL

Kampuni ya Google watambulisha simu mbili mpya, Google Pixel L na Pixel XL. Ujio wa simu hizi ni mwanzo wa mabadiliko makubwa ya biashara ya utengenezaji na uuzaji simu kwa Google.
Baada ya kutoa simu za aina mbalimbali na kuziingiza sokoni kwa jina la ‘Nexus’ Google wafanya mabadiliko makubwa ya utengenezaji simu zao.
Simu za Google Pixel kutoka Google
Tokea mwaka 2010 Google walianza kutoa simu zao za familia ya Nexus lengo likiwa ni kuwaonesha makampuni mengine ya utengenezaji simu yanayotumia programu endeshaji ya Android ni kiwango gani cha ubora kinaweza kufikiwa na simu za familia ya Android.
Na simu za Nexus zimekuwa zikibuniwa na Google na kisha kwa kushirikiana na makampuni mengine kama vile HTC, Huawei na Motorola zimu za Nexus zimekuwa zikija kila mwaka. Sasa Google wanafanya mabadiliko makubwa zaidi, leo huko jijini Calfornia nchini Marekani Google watambulisha vitu kadhaa kikubwa zaidi ikiwa ni simu mpya.
Simu za Google Pixel L na Pixel XL ni simu za ubora wa hali ya juu na hadi sasa zinaweza beba sifa ya kuwa simu za ubora wa juu zaidi kuingia sokoni mwaka huu.
Muonekano
Simu za Google Pixel ingawa zimebuniwa na Google kwa asilimia 100, wameshirikiana na kampuni ya HTC katika utengenezaji wake.
Muonekano wa matoleo yote ya simu za Google Pixel
Utofauti mkuu wa familia hizi mpya za simu kutoka Google ukilinganisha na familia ya zamani, Google Nexus, ni kwamba simu hizi hazibebi alama yeyote kuhusu mtengenezaji (HTC). Zinakuja na alama ya G nyuma yake, ikiwakilisha Google.
Zina jumba (body) lililotengenezwa kwa kutumia alumini (aluminum) na kioo kigumu. Kwa nyuma eneo lote la simu limezungukwa na alumini kasoro eneo dogo la juu lenye sensa ya kamera na kisoma alama za vidole (fingerprint reader).
Simu zote mbili zinakuja katika rangi tatu; rangi ya blu, nyeusi na rangi ya shaba. Wenyewe Google wameita kiutani; ‘Very Silver’, Quite Black na ‘Really Blue’.
Sifa za Undani
Simu hizi zinafanana sifa za undani kwa kiasi kikubwa sana, tofauti kuu ikiwa ni ukubwa wao tuu.
Muonekano (Display)
Google Pixel – inchi 5.0 AMOLED, 1920 x 1080, 441ppi, Gorilla Glass 4
Google Pixel XL – inchi 5.5 AMOLED, 2560 x 1440, 534ppi, Gorilla Glass 4
Prosesa
2.15GHz Qualcomm Snapdragon 821
RAM – GB 4
Ujazo (storage)
GB 32 au GB 128
MicroSD – Hakuna sehemu ya kuweka memori kadi ila ukinunua simu hizi unapata ujazo wa bure (unlimited) wa kuhifadhi picha na video zako kwenye Google Drive.
Kamera
Kamera ya simu za Google Pixels imepata kushinda pointi za kiwango cha juu zaidi kuwahi kutolewa na kampuni inayothaminisha ubora wa kamera – DXOMark
Megapixel 12.3 , f/2.0 aperture, 1.55μm, optical image stabilization, Megapixel 8 (kamera ya selfi)
Tayari simu hizi zishapewa sifa ya kuwa moja ya simu janja zenye teknolojia ya juu kabisa katika ubora wa picha zake. Ni bora kuliko kamera ya iPhone 7 na Samsung Galaxy S7.
Betri
Lisilo toka, mAh 2,770 kwa Pixel L na mAh 3,450 kwa Pixel XL.
Laini
Laini moja katika mfumo wa laini ndogo – NanoSim
Upana na uzito
mm 143.8 x 69.5 x 8.6, gramu 143 kwa Pixel na mm 154.7 x 75.7 x 8.6, gramu 168 kwa Pixel XL.
Zote zinakuja na toleo jipya kabisa la Android, Android 7.1 Nougat, programu endeshaji itaweza kujisasisha (update) bila ata ya kutoa taarifa. Mtumiaji atapewa taarifa ya kuzima na kuwasha simu tuu ili update hizo zimalizie kuwekwa kwenye simu.
Pia simu zote zinauwezo wa kutoharibika pale zikilowa (water resistance). Pia teknolojia ya kisasa kutoka Google kupitia app ya Google Assistant itakuwa inapatikana ndani ya simu hizi.
Pia watumiaji wataweza kupata huduma ya ‘customer care’ masaa 24 . Ukiwa na tatizo lolote katika simu hizo utaweza kupiga screenshot na kutuma na utapewa msaada husika.
Bei na upatikanaji
Kuanzia tarehe 13 walio katika nchi za Marekani, Uingereza, Kanada, Ujerumani, Uingereza na India wataweza kuanza kuilipia mapema ili kujiweka nafasi za mwanzoni kuipata (pre order).
Bei ya Pixel L tole0 la GB 32 ni dola 649 (takribani Tsh 1,410,000/= | Ksh 65,000 ), toleo la GB 32 la Pixel XL ni takribani Tsh 2,000,000.
Kama unataka ujazo wa GB 128 bei itakuwa juu kidogo, Pixel L ni takribani Tsh 1,950,000/= wakati Pixel XL ambayo ni kubwa ni takribani Tsh 2,277,000/=

Previous
Next Post »

Ads Inside Post