TCRA yatoa wiki mbili kwa wadaiwa kulipa madeni yao

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka watoa huduma ambao hawajalipa madeni yao kufanya hivyo haraka kabla Mamlaka haijachukua hatua zaidi za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni na kukabidhiwa kwa kampuni ya kudai madeni.
TCRA imesema tayari watoa huduma 18 waliosimamishiwa leseni zao wameshawasilishwa kwa mdai madeni aliyeteuliwa na Mamlaka ili kukusanya madeni hayo sugu.
Januari mwaka huu, TCRA ilikutana na watoa huduma wenye madeni sugu ya muda mrefu na kuwapa masharti ya jinsi ya kuyalipa madeni hayo haraka ipasavyo na kufanikisha kukusanya madeni ya ada za tozo za Shilingi Bilioni 19.1 hadi kufikia Machi 31, mwaka huu.
TCRA imesema kitendo cha kutolipa ada na tozo za leseni kinasababisha kutokuwepo na ushindani sawa kati ya watoa huduma katika sekta ya mawasiliano na kusababisha kuikosesha serikali mapato yake halali.
Sekta ya Mawasiliano imekuwa kwa kasi nchini ambapo TCRA tayari imekwishatoa leseni 22 za miundombinu ya mawasiliano, leseni 17 za kutoa huduma ya mawasiliano, leseni 85 za huduma za nyongeza za mawasiliano, leseni 154 za huduma za utangazaji ambapo 128 za redio na 26 za Televisheni.

Previous
Next Post »

Ads Inside Post