TAMKO KALI LA SERIKALI KUHUSU TIBA ASILI NA TIBA MBADALA

Ndugu Wananchi, Katika nchi yoyote ile
uhuru usio na mipaka ni jambo la hatari;
lakini pia hakuna haki isiyo na wajibu. Vivyo
hivyo, katika huduma za Tiba Asili na Tiba
Mbadala hapa nchini kuna Sheria, Kanuni na
Taratibu za Maadili zinazoweka masharti,
uhuru na mipaka; pia haki na wajibu wa kila
mdau.
Huduma za tiba asili na tiba mbadala ni
huduma zinazotambulika na Jamhuri yetu,
watu wake na ina thamani kubwa. Aidha, ni
huduma inayotambuliwa na sayansi ya tiba
ya kisasa.
Hata hivyo huduma hizo zimekumbwa na
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuwepo kwa watoa huduma wasiozingatia
Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo na kutokana na ziara
ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt.
Hamisi A. Kigwangalla (Mb) kwa Tabibu
Juma Mwaka Juma tarehe 14/12/2015 na
kufuatia uchambuzi uliofanywa na Wizara
baada ya ziara hii, Wizara imebaini
changamoto zifuatazo:-
1. Huduma za tiba asili na au tiba mbadala
zinatolewa na watoa huduma wasiosajiliwa
na Mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria.
2. Uwepo wa vituo vinavyotoa huduma za
Tiba Asili na au Tiba Mbadala bila kusajiliwa
kwa mujibu wa Sheria.
3. Kutolewa dawa kwa wagonjwa bila dawa
hizo kusajiliwa na mamlaka husika.
4. Uingizaji na matumizi ya vifaa vya
uchunguzi ambavyo havijasajiliwa na
mamlaka zinazohusika, na
5. Utoaji wa matangazo bila ya kufuatwa
kwa matakwa ya sheria, Kanuni na Miongozo
iliyopo. Aidha baadhi ya matangazo hayo
yamekuwa na taarifa zinazoweza kuleta
madhara na kupotosha Umma wa
Watanzania.
Ndugu Wananchi,
Kutokana na hali hiyo, Wizara itahakikisha
kuwa huduma za tiba asili na tiba mbadala
zinatolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
Miongozo iliyopo.
Lengo ni kuwezesha huduma za tiba asili na
tiba mbadala zinakuwa huduma rafiki na
salama kwa watumiaji. Tunao wajibu wa
kuwalinda wananchi, vile vile tunaowajibu wa
kuweka mazingira mazuri kwa watoa huduma
za tiba asili na tiba mbadala ili kufanya
shughuli zao vizuri.
Hivyo kwa upande wetu Wizara itahakikisha
kuwa:-
1. Baraza na sehemu inayosimamia huduma
za Tiba Asili na Tiba Mbadala inakuwa na
watumishi wa kutosha kwa mujibu wa
Ikama.
2. Kunakuwa na Mpango Mkakati wa muda
mrefu kuwezesha kufanikisha uboreshaji wa
huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
3. Watoa huduma wote, vituo vyote vya
kutolea huduma, dawa na vifaa na vifaa tiba
vinavyotumika vinasajiliwa.
4. Utaandaliwa mwongozo wa mafunzo kwa
watoa huduma wote nchini, kuhusu namna
ya kuweka kumbukumbu za wagonjwa, kutoa
rufaa kwa wagonjwa na kutengeneza dawa
zilizo bora.
5. Kunakuwa na mawasiliano na Wizara
zinazohusika na habari na mawasiliano ili
kuboresha utoaji matangazo yanayohusu
Tiba Asili na Tiba Mbadala.
6. Kunakuwa na mawasiliano na Ofisi ya
Rais TAMISEMI na Taasisi za Utafiti ili
kuboresha huduma za tiba asili na tiba
mbadala nchini.
7. Tutafanya mabadiliko ya Sheria ili
kuongeza kiwango cha adhabu kwa
watakaokiuka, na pia tunakusudia kuondoa
Kanuni inayoruhusu matangazo kwa idhini ya
Baraza kwa sababu inaweka mianya ya
matumizi mabaya ya fursa ndogo ya
matangazo inayotolewa.
Ndugu Wananchi, Katika kufanikisha hayo,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto inatoa maelekezo
yafuatayo kwa watoa huduma na jamii:-
1. Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kutoa
huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila
kusajiliwa.
Ninalielekeza Baraza la Tiba Asili na Tiba
Mbadala kuhakikisha kuwa watoaji huduma
wote wanasajiliwa kwa mujibu wa Sheria:
(a) Mijini, (Majiji, Manispaa na Miji) – usajili
wao ukamilike katika kipindi cha miezi
mitatu; kuanzia Januari 15, 2016 na
(b) Vijijini, Halmashauri zote zilizobaki –
usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi
sita kuanzia Januari 15, 2016. Hatua kali za
kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaye
puuza kujisajili katika kipindi hicho
2. Hairuhusiwi kuuza na au kugawa dawa
yoyote ile ya tiba asili au tiba mbadala
mpaka iwe imesajiliwa na Baraza baada ya
kuchunguzwa na Wakala wa Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni salama na
kupewa kibali na Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA).
3. Hairuhusiwi kuendesha kituo cha kutolea
huduma za tiba asili na au tiba mbadala bila
kukisajili.
4. Wizara inapiga marufuku kwa mtu binafsi
au taasisi yoyote ile kutumia kifaa au kifaa
tiba chochote bila kukisajili TFDA na kupewa
kibali; na 5. Matangazo yote yanayohusu
Tiba Asili na Tiba Mbadala ambayo
hayajapitishwa na Baraza yamezuiliwa
kuanzia leo tarehe 15/1/2016.
Wizara inavitaka vyombo vya Habari hasa
Televisheni, Radio na Magazeti kuzingatia
Sheria na Kanuni za Tiba Asili na Tiba
Mbadala inayozuia matangazo ambayo
hayajachunguzwa na Baraza. Ni wajibu wa
vyombo vya habari kujiridhisha na Mamlaka
husika yaani Baraza kabla ya kutoa tangazo
lolote linalohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Wizara itashirikiana na Mamlaka
zinazohusika na habari na mawasiliano
kutekeleza agizo hili. Vile vile, hairuhusiwi
kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya
habari na mikutano ya hadhara kuhusu tiba
asili na tiba mbadala.
Ndugu Wananchi, Katika kuwezesha ulinzi
wa afya za wananchi, kila mmoja wote
alinde afya yake kwa kuhakikisha kuwa
huduma anayopata ya tiba asili na tiba
mbadala ni kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Miongozo inayotolewa na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto.
Ni uhakika uliowazi kuwa kwa pamoja
tukiboresha huduma za tiba asili siyo tu
tutaboresha afya zetu bali pia tutaweza
kuuza dawa na huduma hizo nje ya nchi na
kupata fedha za kigeni kupitia na hivyo
kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja,
jamii na nchi kwa ujumla.
Kwa pamoja tushirikiane kuboresha huduma
za tiba asili na tiba mbadala nchini.
INAWEZEKANA.
Ummy A. Mwalimu (Mb) WAZIRI WA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO 15 Januari, 2016

Previous
Next Post »

Ads Inside Post