Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Ufundi, Dk. Joyce Ndalichako
MWALIMU wa shule ya msingi
Ikombolinga, Peter Emma, ameeleza
masikitiko yake ya kudhalilishwa na
Ofisa Elimu wa shule za msingi,
Mohammed Msongo, wilaya
Chamwino mkoani Dodoma kwa
kumzaba makofi mbele za walimu
wenzake.
Mwalimu Emma anasema
udhalilishaji aliofanyiwa na Ofisa
elimu huyo kwa kupigwa makofi
mbele ya walimu wenzake
unatokana na kuchelewa kufika
katika semina ya mafunzo ya KKK
licha ya kuwa mwalimu huyo
alikuwa anatoka mbali na alikuwa
hajalipwa fedha ya nauli.
Akielezea tukio hilo Mwalimu Emma
amesema kwa mujibu wa ratiba ya
mafunzo ambayo yalianza Januari
16, mwaka huu yalitakiwa kuanza
saa mbili kamili lakini yeye na
wenzake zaidi ya 20 walifika saa
2:40 asubuhi.
Akiendelea kuzungumza na
waandishi wa habari mwalimu huyo
amesema kwamba yeye na walimu
wenzake waliochelewa walimkuta
ofisa elimu huyo na kuwazuia
kuingia darasani kutokana na
kuchelewa kwao.
Amesema Ofisa huyo aliendelea
kuwakaripia na kuwataka waandike
majina yao kwa malengo kwamba
wasihudhurie mafunzo hayo KKK
ambayo yalikuwa yanawahusu
walimu wote wa darasa la kwanza
na la pili.
“Wakati najitetea kuwa tunatoka
mbali na usafiri ni wa shida huku
hatukuwa na fedha, ofisa elimu
alinizaba makofi na kunisukuma
ukutani.
“Kitendo hicho kweli kimeniumiza
na kunidhalilisha sana hata hapa
najifunza lakini sina amani
natamani kurudi nyumbani.
“Tuliandika majina ya waliochelewa
sijui tutalipwa au la maana
tunatakiwa kulipwa Sh. 55,000 kwa
kila siku na nauli lakini mpaka sasa
hatujalipwa mimi sielewi kwa kweli
nimefadhaika sana.
“Kama uongozi ni wa ubabe hivyo
hakika kazi itakuwa ngumu sana
kwani hali hii inavunja moyo,”
amesema Mwalimu Emma.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Chamwino, Richard
Masimba alipotafutwa ofisini kwake
amesema taarifa hizo hawana na
watazifuatilia.
Masimba amesema ofisi haina taarifa
ya mwalimu kupigwa vibao na
kusukumwa ukutani na iwapo
itathibitika hatua za kisheria na
kinidhamu zitafanywa.
Mtuhumiwa wa tukio hilo, Ofisa
Msongo, alipoulizwa alikana na
kukataa katakata kuwa hajampiga
kibao wala kumsukuma ukutani
mwalimu huyo.
“Jumla ya walimu 348 wanapatiwa
mafunzo kazini na mafunzo hayo ni
kwa shule za msingi serikali 119.
“Ila ni kweli wapo walimu
waliochelewa badala ya kufika saa
2:00 kama tulivyo kubaliana wao
wamefika saa 2:40 hivyo walipoteza
dakika 40 za kipindi.
“Kutokana na hali hiyo nililazimika
ukaa na walimu wote waliochelewa
yakiwa makundi mawili na kuwapa
maelekezo ili wasiendelee kuchelewa
kwani kwa kufanya hivyo hawawezi
kufaidika na hayo masomo,”
alijieleza Msongo.
Hata hivyo Msongo amesema siku ya
tukio ambalo inadaiwa alimpiga
mwalimu huyo alimshika shati kwa
nyuma na kumvuta ikiwa ni hatua ya
kutaka asijichanganye na kundi
lingine lisilomuhusu lakini siyo
kumpiga.
Kwa upande wake Katibu wa Chama
cha Walimu (CWT), Wilaya ya
Chamwino, James Puya amesema
analaani vikali kitendo cha ofisa
elimu msingi kumzaba mwalimu
vibao.
“Kitendo hicho kinawafanya
watumishi kukosa morali wa kufanya
kazi kwa ufasaha na wakati
mwingine kuhamishia hasira kwa
watoto.
“Mimi nimepata taarifa za mwalimu
kupigwa na nasema kama kiongozi
wa CWT wilaya ya Chamwino
kulikotokea hili tatizo naomba tume
ya Haki za binadamu, Mkurugenzi
na Utumishi kuingilia kati suala hili.
“Unyanyasaji huu usipokomeshwa
haraka itakuwa mwendelezo wa
viongozi wa ngazi ya juu
kuwanyanyasa watumishi wa ngazi
ya chini jambo ambalo ni hatari,”
amesema Puya.
Next
« Prev Post
« Prev Post
Previous
Next Post »
Next Post »
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
EmoticonEmoticon